Back to top

KIMBUNGA HIDAYA KINASOGEA HUKU KIKIPUNGUA NGUVU - TMA

04 May 2024
Share

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga "HIDAYA" kilichopo karibu na maeneo ya Pwani ya nchi ambapo hadi kufikia saa 9 usiku wa kuamkia leo, Kimbunga "HIDAYA" kilikuwa katika eneo la bahari takribani kilomita 125 kutoka Pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi), kilomita 93 kutoka pwani ya Mafia na kilomita 128 kutoka pwani ya Dar es Salaam kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 985 hPa na kasi ya upepo unaofika kilomita 120 kwa saa.

Taarifa ya TMA imeeleza kuwa tangu usiku wa kuamkia leo, matukio ya upepo mkali na mvua kubwa zinazosababishwa na uwepo wa kimbunga "HIDAYA" yameendelea kujitokeza ambapo hadi kufika saa 3 asubuhi, kituo cha hali ya hewa cha Kilwa Masoko (Lindi) kimeripoti mvua ya jumla ya kiasi cha milimita 111.3 kwa kipindi cha masaa 6 yaliyopita. 

Hata hivyo Kiwango hicho cha mvua ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko ni milimita 96.6 tu. 

TMA imesema kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya saa 24 katika kituo cha Kilwa Masoko ni takribani asilimia 115 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko. 

Viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vingine katika kipindi hicho ni milimita 90.7 kwa Mtwara na milimita 85.3 katika kituo cha hali ya hewa Naliendele (Mtwara). 

Kiwango cha mvua cha milimita 90.7 kilichonyesha Mtwara ndani ya saa 24 ni takribani asilimia 168 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa Mtwara (milimita 54), vipindi vya mvua kubwa bado vinaendelea katika maeneo hayo ya ukanda wa Pwani ya Kusini. 

Hata hivyo TMA imebainisha kuwa katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar, Tanga na Dar es Salaam, upepo mkali unaozidi kilomita 50 kwa saa umeweza kupimwa katika nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi hii.

Aidha, kimbunga "HIDAYA" kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya nchi yetu huku kikipungua nguvu taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 05 Mei 2024.