Independent Television Ltd
Mbunge wa jimbo la Kilombero (CHADEMA) Peter Lijualikali ahukumiwa kwenda jela miezi 6.

Mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Kilombero imemuhukumu kwenda jela miezi sita mbunge wa jimbo la Kilombero kwa tiketi ya  CHADEMA,  Peter Lijualikali(30)   kwa kosa la kufanya fujo na kusababisha taharuki huku aliyewahi kuwa dereva wake,Stephano Mgatta (35) akihukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita.

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu wa mahakama hiyo, Timothy Lyon,  ambaye amedai kutoa adhabu kwa mbunge Lijualikali  ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia ya kufanya makosa ya kujirudia, ambapo amedai  awali mshtakiwa aliwahi kuhukumiwa kesi nyingine tatu tofauti ikiwemo ya oktoba 09 mwaka 2015 alipokutwa na kosa la kumtolea lugha za matusi afisa mtendaji kata ya Ifakara na kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita lakini bado akaonekana kukaidi na kuendelea na makosa hivyo kuonekana mzoefu katika makosa mbalimbali.
 
Hakimu Lyon amedai  mshtakiwa Mgatta, atatumikia kifungo cha nje cha miezi sita kwa vile hilo lilikuwa ni kosa lake la kwanza, na ametakiwa kutotenda kosa lolote ndani ya kipindi hicho cha miezi sita hatotakiwa kutenda kosa lolote la jinai, na washtakiwa hao wamepewa haki na mahakama ya kukata rufaa.
 
Awali imedaiwa na mwendesha mashtaka wa polisi, Inspekta Dotto Ngimbwa kuwa washtakiwa wanadaiwa  kutenda kosa hilo machi mosi mwaka 2016 katika eneo la Kibaoni, katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero, wakati wa zoezi la uchaguzi wa mwenyekiti wa halmashauri na makamu wake ambapo walifanya fujo na kusababisha taharuki na uvunjifu wa amani katika eneo hilo ambapo hata hivyo walikana mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
 
 
Comments
Be the first to comment
ITV SHOWS
Kipima Joto
Utaratibu wa viongozi kukutana na wananchi kusikiliza kero zao. Je, utasaidia kuongeza uwajibikaji kwa watendaji serikalini?
Ndio
Hapana
Sijui
Vote Now
Results
Weather