Independent Television Ltd
Marais wastaafu na mawaziri wakuu wa zamani waongoza waombolezaji kuaga mwili wa Sir.Goerge Kahama Dar es Salaam.

Mwili wa mmoja wa waasisi wa taifa na waziri wa mambo ya ndani wa kwanza Sir.Goerge Kahama umeagwa leo 16 Machi 2017 katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar e s Salaam.

Marais wastaafu na mawaziri wakuu wa zamani ni miongoni mwa waombolezaji walioshiriki kutoa heshima zao za mwisho kabla yakupelekwa kanisa katoliki la mtakatifu Petro Oysterbay kusaliwa na kisha maziko yatakayofanyika makaburu ya kinondoni alasiri leo.
 
MWANASIASA huyo mkongwe na Waziri wa Kwanza wa Ushirika na Masoko katika Baraza la Mawaziri chini ya Serikali ya Madaraka na baadaye Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Ndani baada ya Uhuru, Clement George Kahama `Sir George’ (89) alifariki 12 Mach 2017 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam. 
 
Mtoto wa marehemu, Joseph Kahama alithibitisha kutokea kwa kifo hicho cha baba yake nakusema “Ni kweli, Mzee wetu amefariki dunia saa 10 jioni hapa Muhimbili,” alisema Joseph kwa ufupi.
 
Kahama alizaliwa Novemba 30, 1927 na ameacha mke na watoto 11.
 
Msiba wa Kahama si tu ni mzito kwa familia yake, bali pia kwa taifa kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa kwa nchi kabla na baada ya Uhuru.
 
Kahama ni mtumishi wa umma aliyekuwa mtendaji mkuu na mwanasiasa aliye mahiri na makini katika utendaji kazi kuanzia nyakati za Tanganyika kudai uhuru miaka ya 1950 hadi kujitawala mwaka 1961, na baada ya Uhuru mpaka alipostaafu utumishi wake.
 
Alijiunga na utumishi wa umma baada ya Mwalimu Julius Nyerere kupewa fursa na watawala wa kikoloni mwaka 1958, ya kuunda Serikali ya Madaraka wakiwa na lengo la kuhakiki uwezo wa Watanganyika kujiendeshea nchi yao wenyewe.
 
Wakati serikali hiyo inaundwa, ndipo Mwalimu Nyerere alipomwita Kahama kutoka Bukoba, alikokuwa akifanya kazi katika Chama cha Ushirika cha Kahawa (BCU) ili ajiunge na Baraza la Mawaziri la Serikali hiyo, akamteua kuwa Waziri wa Ushirika na Masoko na mwenyewe (Nyerere) akawa Waziri Mkuu.
 
Baadaye ilipofika Desemba 9, 1961, Tanganyika ilitangazwa kuwa huru, na Baraza la Mawaziri lenye madaraka kamili likaundwa, Kahama akiwa Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
 
Mbali ya nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali, Kahama alipata kuteuliwa kuanzisha taasisi nyeti za kimaendeleo, zikiwa ni pamoja na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Viwanda (NDC); Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA); na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
 
Katika hatua nyingine, Rais John Magufuli alituma salamu za rambirambi kwa familia ya Kahama kutokana na kifo cha kiongozi huyo kilichotokea jana.
 
Katika salamu zake, Rais Magufuli alisema Taifa limempoteza mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kupigania Uhuru, maendeleo na ustawi wa jamii ya Watanzania akiwa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi hususani kuwa miongoni mwa mawaziri katika Baraza la Kwanza la Mawaziri ambapo alishika wadhifa huo kwa awamu tatu za uongozi wa Tanzania.
 
Mwenyezi mungu ailaze roho yamarehemu mahali pema peponi amina.
 
Comments
Be the first to comment
ITV SHOWS
Kipima Joto
Utaratibu wa viongozi kukutana na wananchi kusikiliza kero zao. Je, utasaidia kuongeza uwajibikaji kwa watendaji serikalini?
Ndio
Hapana
Sijui
Vote Now
Results
Weather