Back to top

SERIKALI YAKOSHWA NA UWAMATA KUENDELEZA SEKTA YA MIFUGO

29 April 2024
Share

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefurahishwa na jitihada zinazofanywa na Umoja wa Mapadre Wazalendo nchini (UWAMATA) Jimbo kuu la Mwanza za kuendeleza sekta ya Mifugo kupitia mradi wa  unenepeshaji wa Mifugo ulioanza  kufanyika kwenye eneo la Umoja huo lililopo Kata ya Malya Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza.

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua eneo hilo lenye ukubwa wa takribani Ekari 1200, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti mbali na kuwapongeza viongozi hao wa dini kwa hatua hiyo ameahidi Wizara yake kutoa msaada wa kitaalam wakati wote watakapohitajika kufanya hivyo shambani hapo.

"Mara kadhaa Serikali yetu imekuwa ikishirikiana na Taasisi mbalimbali za dini likiwemo kanisa katoliki katika juhudi mbalimbali za kuwaletea wananchi maendeleo na hili pia tutashirikiana nanyi ili wananchi wanaozunguka shamba hili walitumie kama shamba darasa kwenye dhana ya ufugaji wa kisasa ambao ndio umekuwa msisitizo wetu mkubwa kwa sasa"Ameongeza Mhe. Mnyeti.

Aidha Katika hatua ya kuunga mkono jitihada hizo kwa vitendo, Mhe.Mnyeti ametoa ng’ombe bora 20 kwa Umoja huo ili waweze kuwatumia kuongeza tija kwenye shughuli zao za ufugaji shambani hapo.

Kwa upande wake Mratibu Mkuu wa Mradi huo Padri Samson Masanja ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Malya ameishukuru Serikali kwa kutambua jitihada wanazozifanya ambapo amesema kuwa lengo kuu la mradi ni kuwabadili wafugaji wanaozunguka shamba hilo.

Mradi huo ambao kwa siku za usoni umelenga kuwa kitovu cha uzalishaji wa ng’ombe bora wa maziwa na soko la maziwa yanayozalishwa na wafugaji wanaozunguka shamba hilo umeanza kwa unenepeshaji wa ng’ombe ambapo mpaka sasa kuna ng’ombe 46 wanaonenepeshwa shambani hapo.