Independent Television Ltd
Simba imewatandika JKT Ruvu 2 0 katika ligi kuu ya Vodacom

 Timu ya soka ya wekundu wa msimbazi simba imezidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Vodacom baada ya leo kuwatandika Maafande wa Jkt Ruvu kwa mabao 2-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulianza kwa timu zote kucheza kwa tahadhari kuepuka kufungwa goli la mapema na kusababisha kukosekana kwa mashambulizi ya uhakika lakini iliwachukua Simba dakika 24 tangu mpira kuanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Mrundi Hamis Tambwe kwa njia ya mkwaju wa penati baada ya beki mmoja wa Jkt Ruvu kuunawa mpira katika eneo la hatari wakati akiwa katika jitihada za kuokoa hatari langoni mwake.

Mabadiliko yaliyofanya kocha wa Simba King Abdallah Kibaden mputa ya kumtoa kiungo Amri Kiemba na kumuingiza Kinda Ramadhani Singano Messi katika kipindi cha kwanza yalikuwa na manufaa kwa upande wa wekundu wa msimbasi Simba ambapo dakika tano baada ya mapumziko Singano aliihakikishia Simba pointi tatu muhimu baada ya kufunga bao la pili kwa kumalizika kazi nzuri iliyofanywa na Abdulrahim Humud 'gaucho'.

Kwa ushindi huo Simba imeendelea kukamata usukani wa ligi kuu ya Vodacom kwa kufikisha pointi 14 baada ya kushuka dimbani mara sita huku ikitarajia kushusha tena jeshi lake Oktoba 5 wakati itakapoikabili Ruvu Shooting kwenye uwanja wa taifa.

Comments
Be the first to comment
ITV SHOWS
Kipima Joto
Utaratibu wa viongozi kukutana na wananchi kusikiliza kero zao. Je, utasaidia kuongeza uwajibikaji kwa watendaji serikalini?
Ndio
Hapana
Sijui
Vote Now
Results
Weather