Back to top

ZAIDI YA KILO 767.2 ZA DAWA ZA KULEVYA ZAKAMATWA.

22 April 2024
Share

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imekamata jumla ya Kilogramu 767.2 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, na Tanga kuanzia tarehe 4 hadi 18 Aprili 2024. Kati ya dawa zilizokamatwa, heroin ni kilogramu 233.2, methamphetamine kilogramu 525.67 na skanka kilogramu 8.33. Watuhumiwa 21 wamekamatwa kuhusika na dawa hizo za kulevya, baadhi yao wamefikishwa mahakamani na wengine watafikishwa taratibu za kisheria zitakapokamilika.

Operesheni zilizofanikisha ukamataji huu ni kama ifuatavyo: Tarehe 04 Aprili, 2024, eneo la Mikanjuni jijini Tanga watuhumiwa wawili walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha gramu 329.412. Tarehe 08 Aprili, 2024, eneo la Wailes Temeke mtaa wa Jeshini, jijini Dar es Salaam zilikamatwa kilogramu 1.49 za dawa za kulevya aina ya skanka ambapo watuhumiwa wawili walikamatwa kuhusika na dawa hizo.

Katika operesheni iliyofanyika tarehe 10 Aprili, 2024, eneo la Zinga Bagamoyo mkoani Pwani, zilikamatwa kilogramu 424.84 za dawa ya kulevya aina ya methamphetamine. Watuhumiwa watatu walikamatwa kuhusika na dawa hizo. Tarehe hiyohiyo katika eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam, alikamatwa mtuhumiwa mmoja akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha gramu 158.24. Tarehe 14 Aprili, 2024 eneo la bandari jijini Dar es Salaam zilikamatwa kilogramu 4.72 za dawa za kulevya aina ya skanka.

Watuhumiwa watatu walikamatwa kuhusika na dawa hizo. Aidha, tarehe 16 Aprili, 2024 katika kata ya Kunduchi jijini Dar es Salaam zilikamatwa kilogramu 232.69 za dawa za kulevya aina ya heroin na kilogramu 100.83 za dawa ya kulevya aina ya methamphetamine zilizokuwa zinaingizwa nchini kupitia Bahari ya Hindi. Watuhumiwa tisa waliokamatwa katika tukio hili. 2 Vilevile, tarehe 18 Aprili, 2024 mtuhumiwa mmoja alikamatwa eneo la bandari jijini Dar es Salaam akiwa na kilogramu 2.12 za skanka.

Baadhi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya wameendelea kutumia vifungashio vyenye majina ya aina mbalimbali ya kahawa na chai kama vile organic coffee, cocoa, na green tea kwa lengo la kukwepa kutiliwa mashaka wakati wa kusafirisha dawa za kulevya. Biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni moja ya matishio makubwa kiusalama duniani hasa ikizingatiwa kuwa, vijana ndio kundi linaloathiriwa zaidi na dawa hizo. Kwa mujibu wa takwimu ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, idadi ya vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa ni 20,612,560 sawa na wastani wa 50% ya idadi ya watu wote nchini Tanzania.

Kati ya watuhumiwa wanaokamatwa, wengi wao wako katika kundi la vijana. Ikiwa kundi hili litaendelea kujiingiza kwenye biashara na matumizi ya dawa za kulevya litapoteza ustawi binafsi, Taifa litapoteza nguvu kazi na hatimaye kuhatarisha uchumi na usalama wa Taifa letu. Ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatoa shukrani kwa wadau wote wakiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na Mamlaka kwa namna moja ama nyingine kufanikisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Pia, tunawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa kupiga namba yetu ya bure 119.