Back to top

ACT Wazalendo wahoji chanzo cha polisi kukamata maafisa wake watatu.

26 September 2020
Share

Chama cha ACT Wazalendo kimelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja au kuwafikisha mahakamani kama kuna kosa lolote wamelifanya. Maafisa watatu wa chama hicho waliokamatwa jana katika ofisi za chama hicho magomeni jijini Dar es salaam.

Chama hicho kimesema kuwa wanachama wake watatu akiwemo Afisa Habari Mwandamizi Dotto Rangimoto,  Afisa uchaguzi Dahlia Majid na Arodia Peter ambaye ni Afisa Habari Uenezi wanashikiliwa na Jeshi la Polisi bila kupewa sababu za kushikiliwa kwao.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema ni kweli amepata taarifa za Maafisa wa ACT kukamatwa lakini yeye hana taarifa za kwanini wamekamatwa kwakuwa yeye sio muhusika wakulijibu hilo.

Kufuatia taarifa ya chama hicho iliyoandikwa na Katibu Idara ya Habari,Uenezi na mahusiano kwa Umma Septemba 26 imesema chama kupitia mwanasheria wake kimetumia jitihada mbalimbali kushughulikia taratibu za dhamana ila imeshindikana.

Taarifa imesema maafisa hao walikamatwa wakati wakiwa kwenye majukumu yao katika Ofisi za chama Magomeni jijini dar es Salaam Septemba 25, 2020.