Back to top

Adaiwa kufariki baada ya kutumbukia mtoni akiwakimbia polisi.

04 November 2019
Share

Wafugaji wa kijiji cha Mkunywa, kata ya Madibira wilayani Mbarali wameiomba serikali kuwasaidia kuchunguza kifo cha mtoto Jidamabi lwenge (15) ambaye anadaiwa kufariki kwa kutumbukia mtoni wakati akiwakimbia askari polisi ambao walikuwa wanamfukuza ili wamkamate kwa tuhuma za kunywesha mifugo jirani na mashamba ya mpunga ya ushirika wa Madibira.

Wafugaji jamii ya Wasukuma, wakazi wa kata ya Madibira wilayani Mbarali, wameiomba serikali kuingilia kati unyanyasaji wanaofanyiwa na Jeshi la polisi wilayani humo wakidai kuwa askari wa Jeshi la polisi wamekuwa wakitumia bunduki kuwatisha na kisha kukamata mifugo yao wanapokwenda kunywesha maji katika mto Lwandembela ili wawatoze faini, kitendo ambacho wanadai kuwa sasa kimesababisha kifo cha mtoto Jidamabi Lwenge aliyefufa maji baada ya kutumbukia mtoni wakati akiwakimbia askari hao.

Katibu wa chama cha wafugaji wilaya ya Mbarali, Matagili Mbigili, amewataka wafugaji hao kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho wanafuatilia tatizo hilo, akidai kuwa serikali ya awamu ya tano ni sikivu na inao uwezo wa kushughulikia tatizo lao.

Akizungumza na ITV kwa njia ya simu, Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Kamishna msaidizi mwandamizi wa Jeshi la polisi, Ulrich Matei amesema hana taarifa ya tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa kuhusu tukio hilo baada ya kuwasiliana na mkuu wa polisi wilaya ya Mbarali.