Back to top

Aliyehusika na mauaji ya kikongwe Rombo 2017 akamatwa baada ya miaka 3

09 October 2020
Share

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limefanikiwa kumtia mbaroni mtu anayeshukiwa kuwa jambazi Luka Kavishe wa kijiji cha Mbomai wilayani Rombo kwa kuhusika na mauaji ya kikatili ya marehemu Febronia Mangowea wa kijiji hicho miaka mitatu iliyopita.

Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro kamishna msaidizi wa Polisi Emmanuel Lukula amesema, mauaji hayo yalifanyika julai 31 mwaka 2017 saa moja na nusu usiku katika shamba la marehemu katika kijiji hicho na kukamatwa mwaka huu katika eneo la kata ya pasua manispaa ya Moshi.

Kamamda Lukula amesema, kabla ya kifo chake marehemu alibakwa kinyama na mtuhumiwa kwa imani za kishirikina ambazo kamanda amezikemea na kueleza kuwa hazihusiani na mambo ya ushirikina.

Mtoto wa Marehemu Bi.Teddy Tesha amewapongeza polisi wa vituo vya Tarakea, mkuu Rombo na Moshi mjini kwa ushirikiano nzuri uliofanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa ambaye alitoroka baada ya mauaji hao miaka mitatu iliyopita.