Back to top

Ardhi iliyomilikiwa WaKenya kabla ya kuwekwa mipaka kutaifishwa.

10 June 2018
Share

Serikali imetangaza kuwa ardhi yote ambayo imekuwa ikitumiwa na Raia wa nchi ya Kenya kabla kuwekwa kwa mipaka ya kutenganisha nchi hizi mbili itamilikiwa na serikali ya Tanzania na kwamba raia wote wa Kenya wataruhusiwa kutumia ardhi hiyo kwa kufuata taratibu na sheria wakiwa kama wawekezaji na si vinginevyo.

Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya makazi Mh William Lukuvi,ametangaza uamuzi huo katika kijiji cha Nyakarima wilayani Tarime mkoani Mara muda mfupi baada ya kukamilisha zoezi la ukaguzi wa uwekaji wa vigingi vya kutenganisha mpaka ya nchi ya Kenya na Tanzania kwa upande wa mkoa wa Mara.


Hata hivyo kiongozi huyo mwenye dhamana na ardhi, amewaonya viongozi wote wa serikali za vitongoji,vijiji na kata kuacha mara moja kuwafukuza watu ambao tayari wanakalia ardhi ya Tanzania  baada ya kuwekwa kwa alama hizo za mipaka kwa maelezo kuwa zoezi hilo la kuwandoa litafanyika kwa amri za marais wa nchi hizi mbili.

Naye Mkuu wa mkoa wa Mara Bw Adam Ally Kighoma Malima,ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, ameviagiza vyombo vya dola  kuchukua hatua kali kwa watu watakaobainika kuharibu vigingi hivyo ambavyo vimewekwa kwa gharama kubwa kwa ajili ya kutenganisha nchi hizi mbili.