Back to top

Atakayeshindwa kumilikishwa 'ardhi' ndani ya miezi 3 kudaiwa kodi.

12 August 2020
Share

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Angeline Mabula amezitaka idara za Ardhi katika halmashauri nchini kutoa elimu kwa wamiliki wa ardhi kuhusu sheria mpya ya fedha inayowataka wamiliki waliokamilisha taratibu zote za kumilikishwa ardhi kuchukua hati ndani ya siku tisini.

Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi kwenye halmashauri za wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Bukoba, Muleba na Biharamulo mkoani Kagera katika ziara yake ya kikazi, Mhe.Mabula amesema sheria ya fedha namba nane ya mwaka 2020 iliyotoa mabadiliko katika vifungu namba 24 na 33 vya sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 inataka wamiliki ambao michoro yao imeidhinishwa waombe kumilikishwa ndani ya siku tisini na wasipofanya hivyo wataanza kudaiwa malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi kuanzia pale michoro ilipopitishwa.

Naibu Waziri Mabula amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kwenye halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatoa elimu kwa kutumia njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari ili wananchi waombe kumilikishwa kuepuka kuumia baadaye kwa kudaiwa malimbikizo ya kodi ya ardhi.

Kwa mujibu wa Mhe.Mabula, mmiliki wa ardhi atakayeshindwa kuomba kumilikishwa ama kupatiwa hati ndani ya miezi mitatu basi ataanza kudaiwa kodi ya ardhi kuanzia pale mchoro wake ulipopitishwa hata kama ulipitishwa mwaka 1990 jambo alilolieleza litamgharimu mmiliki kulipa kiasi kikubwa cha fedha.

"Sheria inawataka wenye approved survey waombe kumilikishwa ndani ya siku tisini na wakichelewa kuomba basi wataanza kudaiwa kuanzia pale mchoro ulipopitishwa maana serikali imeingia gharama kubwa katika upimaji"Mhe.Mabula

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kuwa, sheria hiyo ya fedha ilipitishwa na Bunge Julai 2020 na kufikia mwezi Oktoba mwaka huu itakuwa mwisho kwa wale ambao michoro yao imepitishwa kudai hati na kitakachofuata ni .kupelekewa hati za madai ya kodi ya pango la ardhi na kusisitiza ni vizuri kipindi kilichobaki wamiliki wakajitokeza kumilikishwa mapema.

Katika ziara yake hiyo Mhe.Mabula aliwataka pia watendaji wa sekta ya ardhi kuhakikisha maeneo yote ya umma yanapimwa na kupatiwa hati sambamba na vijiji kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Angeline Mabula yuko katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Mara, Kagera, Mwanza, Shinyanga na Tabora kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi, kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi, kugawa hati za ardhi  pamoja na kukagua miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).