Back to top

AU kujenga Kituo cha kimataifa cha Huduma za mawasiliano Arusha

07 December 2018
Share

Tanzania imetoa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kimataifa cha huduma za mawasiliano kinachojengwa Jijini Arusha kitakachosimamiwa  na Umoja wa Nchi za Afrika (AU).

Mwakilishi wa AU Bw.Kolowole Adowoje amesema tayari wameshapokea hati ya umiliki wa aridhi hiyo na mchakato wa kuanza ujenzi wa kituo hicho umeshanza na kwamba pia kinatarajiwa kuwa makao makuu ya mashirika ya posta barani afrika.

Meya wa Jiji la Arusha Mstahiki Kalst Lazaro amesema taratibu za kukabidhi eneo hilo kwa watendaji wa AU zimeshafanyika na amezishukuru taasisi na idara za serikali kwa kuharakisha mchakato huo.

Akizungumza baada ya kukutana na wadau wa mawasiliano na huduma za posta kutoka nchi mbalimbali za afrika Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mh Issack Kamwelwe amesema hatua hiyo itaendelea kurahisisha mawasiliano kitaifa na kimataifa.

Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mh Issack Kamwelwe

Katika hatua nyingine Waziri Kamwelwe amesema pamoja na kupanua mtandao wa huduma za mawasiliano pia serikali inaendelea kufanyia kazi malalamiko ya wananchi dhidi ya baadhi ya kampuni zinazokiuka sheria za huduma za mawasiliano na kuwaumiza wananchi.