Back to top

Basi lenye uwezo wa kubeba watu 60 lakamatwa likiwa na abiria 100. 

09 July 2019
Share

Basi  lenye uwezo  wa kubeba abiria  60 linalofanya safari  zake kuanzia Arusha kwenda  kiteto mkoani Manyara limekamatwa  na polisi likiwa limebeba abiria zaidi  ya 100 kitendo kinachodhihirisha jinsi baadhi  ya madereva na makondakta wanavyochezea maisha  ya watu na kukiuka sharia.

Akizungumzia  tukio hilo Kamanda  wa kikosi cha usalama  barabarani mkoa wa Arusha Bw  Joseph Bukombe amesema kukamatwa  kwa basi hilo lenye namba za usajili  T 945 AAU la kampuni ya Kimotco hayo ni matokeo  ya operesheni ya kufuatilia mabasi yote yanayokwenda  mikoani inayoanywa na kikosi maalumu cha polisi inayolenga  kukomesha ukiukwaji wa sharia unaoendelea kufanywa na baadhi ya  madereva na pia baadhi ya askari wasio waaminifu.

Wakati  kondakta wa  basi akidai kuwa waliokuwa  wamezidi kwenye basi ni wanafunzi  na walimu na baadhi ya abiria wakidai kuwa  wanalazimika kupanda magari yaliyojaa kutokana na uhaba  wa mabasi , mmiliki wa basi hilo Bw Benedikti Mberesero  amesema yeye hajawatuma dereva na kondakta wake kuvunja sheria  na kwamba kitendo walichofanya hakikubaliki na yeye hakiungi mkono.