Back to top

Bodi ya Mazao Mchanganyiko kununua korosho zote za wakulima.

07 December 2018
Share

Waziri Mkuu Mh.Kassim Majaliwa amewatoa hofu wananchi hususani wakulima wa korosho nchini na kusema serikali kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko itanunua korosho zote na hakuna korosho za wakulima nchini ambazo zitabaki bila ya kununuliwa.

Kauli hiyo ameitoa alipozungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha korosho cha Terra akiwa njiani kwenda Dodoma, na kueleza kuwa bodi hiyo inaendelea kufanya thamini na kujiridhisha kama kweli korosho hizo zimezalishwa nchini na kuangalia viwango vya ubora na baada ya kujiridhisha kuhusu viwango vya ubora na mkulima aliyepeleka ndiye mwenyewe ndipo taratibu za malipo hufanyika.

"Lengo la Serikali ni kuhakikisha mkulima ananufaika na ndipo Rais Dkt. John Magufuli alisitisha ununuzi baada ya kuona wakulima wanataka kudhulumiwa."

Waziri Mkuu amesema kuwa hadi sasa tayari tani 181,000 zimeshakusanywa, hivyo amewataka wakulima wa zao hilo nchini waendelee kuiamini Serikali yao.

Kwa upande wake Meneja Utawala wa kiwanda cha Terra, Peter Ngwale alisema uwezo wao ni kubangua tani 6,000 kwa mwaka, ambapo tayari wamebangua tano 3,000.

Pia aliiomba Serikali iwasaidie katika suala la ubora wa korosho kwa kuwa kiwango cha ubora kinachoandikwa kinakuwa tofauti na uhalisia wa korosho yenyewe.