Back to top

Chama cha wakandarasi wazawa kumburuza Mahakamani Mhe.Ndugulile

10 January 2019
Share

Chama cha wakandarasi wazawa nchini kimesema kinakusudia kumshtaki mahakamani naibu waziri wa afya, Dkt.Faustine Ndugulile kutokana na tamko lake alilolitoa hivi karibuni mkoani Ruvuma la kupiga marufuku watendaji wa halmashauri zote nchini kutumia wakandarasi kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya sekta ya afya.

Rais wa chama cha wakandarasi wazawa nchini, Kura Mayuma ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wandishi wa habari jijini Mbeya akidai kuwa agizo hilo la naibu waziri wa afya, Dkt.Faustine Ndugulile linavunja sheria ya usajili ya wakandarasi ya mwaka 1997.

Pamoja na kusudio hilo, Mayuma amesema kuwa wakandarasi nchini hawana ugomvi na serikali, hivyo kama naibu waziri huyo atafuta kauli yake hadharani hawatakuwa na sababu ya kuelekea mahakamani kushimtaki.

Baadhi ya wakandarasi wamesema kuwa serikali kupitia baadhi ya halmashauri zake nchini imekuwa ikiwatumia mafundi wa mitaani kupitia utaratibu wa force account kutekeleza miradi ya ujenzi na kudai kuwa utaratibu huo unapunguza gharama na kuokoa fedha, jambo ambalo sio sahihi kutokana na utaratibu huo wa force account kutolipa kodi na gharama nyingine wanazolipa wakandarasi.

 Hivi karibuni akiwa mkoani Ruvuma katika ziara yake ya kikazi, naibu waziri wa afya, Dkt. Faustine Ndugulile aliwaagiza watendaji wa halmashauri zote nchini kutowatumia wakandarasi kutekeleza miradi ya sekta ya afya na badala yake miradi hiyo itekelezwe kwa utaratibu wa force account.