Back to top

Dawa za majaribio ya kutibu Ebola zaonesha mafanikio Kongo.

13 August 2019
Share

Wizara ya Afya katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo imesema dawa mbili za majaribio ya kuutibu ugonjwa wa Ebola zinaonekana kuyanusuru maisha ya wagonjwa. 

Dawa hizo zinazotokana na kingamwili za watu walionusurika ugonjwa huo hatari zimeonyesha mafanikio mema miongoni mwa wagonjwa waliozitumia, katika juhudi za kupambana na mlipuko wa sasa wa Ebola Mashariki mwa Kongo. 

Aina nne za dawa zilikuwa zikifanyiwa majaribio, lakini aina mbili, REGN-EB3 na mAb114 zilionekana kuleta matokeo bora. 

Nyingine mbili, ZMapp na Remdesivir sasa zimeachwa kutumiwa. Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimarekani kwa ajili ya magonjwa ya kuambukiza Antony Fauci amesema mafanikio ya dawa hizo ni habari njema, ambazo zinaashiria kupatikana kwa tiba dhidi ya maradhi ambayo mnamo kipindi cha hivi karibuni ilikuwa hata haifikiriki. 

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limewahimiza wagonjwa wa Ebola kutafuta dawa hizo haraka.

DW.