Back to top

Dodoma yaingia makubaliano na TFS kuhifadhi mazingira na misitu

12 July 2018
Share

Halmashauri ya jiji la Dodoma limeingia makubaliano na wakala wa huduma za misitu nchini TFS kwaajili ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira na misitu yote ndani ya jiji hilo ikiwa ni hatua ya kuendeleza program ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani iliyozinduliwa na makamu wa rais Mhe.Samia Suluhu Hassan mwezi Desemba mwaka jana.

Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Godwin Kunambi akiongea baada ya kutiliana saini makubaliano ya kisheria  na wakala wa huduma za misitu nchini TFS kuifanya Dodoma kuwa ya kijani amesema mpango huo unalenga kuboresha mazingira ya jiji na kwamba kuanzia sasa jiji litakabidhi vilima vyote kwa TFS ili vihifandhiwe kisheria na kuepuka wavamizi ambao wanataka kuharibu mazingira ya jiji kwa shughuli zao binafsi.

Nae mtendaji mkuu wa wakala wa huduma za misitu nchini TFS Profesa Dosantos Silayo akiongea baada ya kutembelea msitu wa hifadhi wa Mahomanyika ambao ni miongoni mwa maeneo ya kipaumbele kwa uhifadhi jiji la Dodoma amesema TFS imetenga zaidi ya shilingi milioni 300 kwaajili ya kutekeleza mipango ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani ikiwemo upandaji wa miti na uhifadhi wa misitu ya asili.

Afisa misitu wa jiji la Dodoma Bwana Salvatory Mashamba amesema msitu wa hifadhi wa Mahomanyika uliokuwa na ukubwa wa zaidi ya hekta elfu saba umeharibiwa kutokana na ongezeko la shughuli za binadamu na wavamizi lakini kupitia makubaliano hayo ya kisheria uhifadhi wa msitu huo utaimarika zaidi.