Back to top

Hakimu amtaka Katibu mkuu wa CHADEMA kufika mahakamani kujieleza.

16 April 2019
Share

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemtaka Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt.Vicent Mashinji kwenda kujieleza mahakamani kwanini ameshindwa kuhudhuria kesi yake iliyopo mahakamani hapo.

Dkt.Mashinji ambaye ni mshtakiwa wa sita katika kesi ya kufanya mkusanyiko usiohalali, inayowakabili yeye na vigogo wenzake tisa wa chama,ameshindwa kufika mahakamani hapo kwa maelezo kuwa yupo kwenye kesi nyingine iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea.

Dkt.Mashinji ametakiwa kwenda kuieleza mahakama hiyo, April 17, mwaka huu sababu za yeye kushindwa kufika mahakama hapo, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.

Dkt.Mashinji na wenzake wanakabiliwa na makosa 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, February 1 na 16, 2018, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko la kutawanyika.