Back to top

Halmashauri za wilaya zaagizwa kutoza tozo kisheria

10 August 2018
Share

Halmashauri za wilaya zenye machimbo ya aina yoyote ya madini nchini zimeagizwa kuweka sheria ndogo ya kuwatoza tozo zinazozingatia sheria wawekezaji wa ndani na nje watakaochimba madini hayo ili kujiepusha na migogoro kati ya halmashauri hizo na wawekezaji.

Naibu waziri wa madini Mhe.Dotto Biteko amesema, kutokuwepo kwa sheria zinazotambuliwa rasmi kisheria kwa baadhi ya halmashauri za wilaya kumekuwa kukiwakatisha tamaa wawekezaji na hivyo kuikosesha  serikali mapato ambayo yangesaidia kuboresha huduma za kijamii.

Mhe. Biteko ametoa agizo hilo wakati alipotembelea machimbo ya udongo yenye madini aina ya Bauxite ya kampuni ya kizalendo ya Willy Enterprises katika milima ya Shengena wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Mhandisi John Mhagama wa kampuni hiyo amesema, huduma za uchimbaji na usaifirishaji wa udongo huo imesimamishwa wakati ikisubiri mwongozo kutoka serikalini baada ya serikali kusimamisha usafirishaji wa madini ghafi kwenda nje ya nchi.
 
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Same Bi.Rosemary Senyamule amesema, kampuni hiyo imekuwa ikifanya shughuli zake kwa kuzingatia hifadhi ya mazingira bila kuleta athari  katika uhifadhi ya mazingira.