Back to top

Hasunga aiagiza bodi ya pamba kutayarisha vitambulisho vya wakulima.

17 July 2019
Share

Waziri wa Kilimo Mhe.Japhet Hasunga ameiagiza bodi ya Pamba nchini kutayarisha vitambulishio vya wakulima wa zao la Pamba wote nchini na kuvigawa bure kwa lengo la kuwatambua huku akiwatoa hofu juu ya soko la pamba na kuviagiza vyama vya msingi kuhakikisha ifikapo tarehe 30 ya mwezi huu pamba yote ya wakulima iwe imeshanunuliwa na wamelipwa fedha zao.

Mhe.Hasunga ametoa kauli hiyo katika ziara yake ya kukagua na kufuatilia mwenendo wa ununuzi wa zao la Pamba kutoka kwa wakulima mkoani Shinyanga ambapo amewatoa hofu wakulima na kuahidi kuwa serikali imeamua kufidia kiasi cha fedha kwa wanunuzi ili waanze kununua pamba kwa bei ile ile ya shilingi 1,200 kwa kilo.

Awali akiwa katika ziara baadhi ya wakulima wamelalamikia kutolipwa fedha zao tangu wauze pamba kwa baadhi ya wanunuzi na kumuomba waziri kupokea kilio chao na kuchukua hatua ili kuwanusuru na hali ya njaa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote pamoja na madiwani kuwasimamia wananchi na kuhakikisha wanapouza mazao yao ikiwemo pamba kujiunga na bima ya afya ili kupunguza changamoto ya kutumia gharama kubwa katika matibabu ili fedha zitumike katika miundombinu ya kujiongezea kipato.