Back to top

Hoja 5 za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi zafutwa.

17 October 2020
Share

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimetia saini hati za makubaliano kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi.

Hoja hizo ni Ushirikishwaji wa Serikali ya Mapinduzi yaZanzibar kwenye masuala ya kimataifa na kikanda, Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Gharama za kushusha mizigo bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar, Utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi na Utaratibu wa vikao vya kamati ya pamoja ya serikali hizo ya kushughulikia masuala ya Muungano.

Makubaliano yaliyofikiwa Ikulu jijini Dar es Salaam yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali hizo mbili akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta Hussein Mwinyi pamoja na Wanasheria Wakuu wa serikali wa pande zote mbili za Muungano.

Akizungumza katika hafla hiyo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, amesema serikali inazifanyia kazi hoja zote zitakazoletwa na hadi sasa hoja tano zimepatiwa ufumbuzi na kusainiwa.

Amesema hizo zitaenda kuhamasisha uwajibikaji, kudumisha ushirikiano kati ya pande zote mbili za Muungano pamoja na kupelekea maendeleo yatakayo wezesha kukua kwa uchumi.