Back to top

ICC yamkuta na hatia kiongozi wa zamani wa waasi Congo, Bosco Ntaganda

08 July 2019
Share

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imemkuta na hatia Kiongozi wa zamani wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bosco Ntaganda kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu katika eneo la Ituri, mashariki mwa DRC.

Majaji walimkuta na hatia Ntaganda kwa makosa 18 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu uliotokea katika mji wa mashariki wa Ituri mwaka 2002 na 2003.

Ntaganda, 45, ''kiongozi mkuu'' alikuwa akitoa amri ''kuwalenga na kuwaua raia'' Jaji Roberrt Fremr amesema kwenye hukumu .

Waendesha mashtaka wamesema Ntaganda alipanga na kuongoza operesheni ya waasi wa Union of Congolese Patriots (UCP) na tawi lake la kijeshi, la Patriotic Forces for the Liberation of Congo (FPLC).

Amekutwa na hatia kuhusika na vitendo vya ubakaji na utumwa wa kingono. Majaji pia wamesema Ntaganda mwenyewe alimuua kasisi wa kikatoliki.

Uhalifu huu ulifanyika wakati Ntaganda alipokuwa kiongozi wa kundi la waasi lililokuwa chini ya Thomas Lubanga, kiongozi wa waasi wa UPC. Alihukumiwa na ICC mwaka 2012.

Majaji wamemkuta na hatia Ntaganda kwa uhalifu wa kuwasajili watoto kwenye jeshi, wakiwemo wasichana.