Back to top

Kabudi atoboa siri alivyoandika barua ya kujiuzulu ikachanwa.

24 January 2020
Share

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi ametoboa siri mbele ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli namna alivyoandika barua ya kujiuzulu kwenye nafasi yake na kuzuiwa na 'Kasmir Sumba Kiuke', baada ya mchakato na wajumbe wa Barrick kuwa mgumu nakuona ni aibu kushindwa kazi aliyotumwa na Mhe.Rais.

"Mhe.Rais niliandika barua ya kujiuzulu kuja kwako, kwamba kazi uliyonipa nimeshindwa , aibu hii na fedheha hii nitaibeba, barua hiyo sikuileta 'Kasmir Sumba Kiuke' alininyang'anya akaichana"-Waziri Kabudi. 

Prof.Kabudi ametoa kauli hiyo  wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano kati ya serikali na kamati ya madini ya Barrick.

Prof.Kabudi akizungumza mbele ya Rais Magufuli ameeleza kwamba hapendi kuwataja watu majina ambao walitia vikwazo wakati wa mchakato wa kuhakikisha kwamba mikataba hiyo inasainiwa ili kuweza kuleta manufaa kwa taifa, huko Toronto na London kwani kila walipokutana na kukubaliana kesho yake walibadili njia.

“Kuna wakati walikuja Wachina tofauti wa kuwekeza tukaongea nao ila wakaingia mitini, huku bungeni unapigwa mijeledi, huku Wachina wale wameingia mitini, huku rais anasubiri umalize, huku unajiuliza utatoka kwa aibu ila Mungu akasimama na sisi,”Profesa Kabudi.

Prof.Kabudi ameongeza kuwa wakati wa majadiliano kati ya Tanzania na Barrick Prof. John Thornton alikubali mikataba haikuwa mizuri na lazima irekebishwe, na Rais Magufuli alisema sitaki mikataba irekebishwe kwa ajili yangu, fedha yote itakayopatikana itakwenda kwenye shule, afya, miundombinu .
Hii ndio Mikataba 9 iliyosainiwa Kati ya Tanzania na Barrick.

  1.  Mkataba wa Msingi wa Makubaliano
  2.  Mkataba wa Menejimenti na Utoaji Huduma
  3. Mkataba wa Wanahisa wa Kampuni ya Twiga
  4.  Mkataba wa wanahisa wa Kampuni ya North Mara
  5.  Mkataba wa wanahisa wa Kampuni ya Bulyankulu
  6.  Mkataba wa wanahisa wa Kampuni ya Buzwagi
  7.  Mkataba wa maendeleo wa Mgodi wa North Mara
  8.  Mkataba wa maendeleo ya Mgodi wa Bulyankulu
  9.  Mkataba wa maendeleo ya Mgodi wa Pangea