Back to top

Kabudi:Tanzania inaheshimu na itaendelea kuheshimu haki zote binadamu.

26 February 2020
Share

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.Palamagamba Kabudi ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania  inaheshimu na itaendelea kuheshimu haki zote binadamu zikiwemo za kisiasa na kwamba sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zina lengo jema la kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa Taifa lenye amani,umoja na utulivu.

Akihutubia katika Kikao cha 43 cha Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa linaloendelea Geneva nchini Uswisi Prof.Kabudi amesema hatua zote ambazo zimechukuliwa na Bunge la Tanzania kwa kufanya mabadiliko katika sheria za vyama vya siasa,sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali na ile ya vyombo vya habari ina lengo la kuimarisha uwajibikaji na uwazi pamoja na kuhakiskisha misingi na tunu za Taifa zinaheshimiwa na kuendelezwa.

 
Pia Prof. Kabudi ameifahamisha jumuiya ya Kimataifa kuwa mwaka huu Tanzania itafanya uchaguzi wake mkuu wa sita tangu kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa na kuihakikishia jumuiya hiyo kuwa uchaguzi huo utakuwa wa uwazi,huru na wa haki na kwamba Tanzania itaalika waangalizi mbalimbali wa uchaguzi watakaotaka kushuhudia namna Watanzania wanavyotekeleza moja ya haki zao za msingi katika suala la kidemokrasia  kwa kuchagua viongozi wao.