Back to top

Kamati za Maafa zatakiwa kuungana kukabiliana na Corona.

27 March 2020
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ameziagiza kamati za Maafa katika ngazi za mikoa na wilaya ziungane na waratibu wa kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona waliopo katika maeneo yao.

Amewasisitiza Watanzania waendelee kujikinga na ugonjwa huo kwa kuhakikisha wanajiepusha na misongamano isiyokuwa ya lazima na hata wakienda kwenye maeneo ya kutolea huduma kama sokoni, vituo vya mabasi wapeane nafasi kati ya mtu mmoja na mwingine.

Ametoa maagizo hayo jijini Dodoma katika kikao cha Kamati ya Kitaifa cha Kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipeleke wataalamu katika maeneo yenye mahitaji makubwa kama kwenye viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na bandarini.

Ameitaka kamati hiyo ifuatilie na isimamie vizuri ili kuhakikisha watu wote wanaoingia nchini wanapimwa na wanafuatilia ili kujua historia zao za safari katika kipindi cha siku 14, lengo likiwa ni kuzuia maambukizi hayo yasisambae kwa jamii, Kikao hicho kimehusisha wajumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.