Back to top

Kambale wadogo walioingizwa nchini kimagendo wanaswa Kagera.

11 April 2019
Share

Samaki wadogo aina ya kambale ambao wavuvi huwatumia kama chambo kuvulia samaki aina ya sangara wamekamatwa katika eneo la Kemondo wilayani Bokoba mkoani Kagera wakati  wakisafirishwa kwenda kwenye mkoani Geita ambao inadaiwa samaki hao wameingizwa nchini toka nchi jirani ya Uganda kwa kutumia njia za panya.

Samaki hao walikuwa wamehifadhiwa kwenye madumu 56 yenye ujazo wa lita 20 na walikuwa wakisafirishwa kwa gari aina ya Canter yenye namba za usajili T 989 DPP.

Afisa wa  idara ya uvuvi katika halmashauri hiyo, Lewis Luhuzi amesema samaki hao walikuwa wanasafirishwa bila vibali na wamezalishwa kwenye mabwawa yaliyoko nchini Uganda hata hivyo kauli hiyo imepingwa na  Wilson Mwita aliyekamatwa na samaki hao aliyesema amewapata kutoka ndani ya mto Kagera.

Afisa Uvuvi wa mkoa wa Kagera Efraz Mkama  ametoa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kusafirisha samaki au mazao ya samaki kinyume na taratibu zilizowekwa, amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wanaojihusisha na vitendo hivyo kwa kuwa misako inayofanyika mkoani humo ni endelelevu.