Back to top

Kanyasu atoa miezi 3 kwa wananchi waliovamia Shamba la miti Biharamulo

22 March 2019
Share

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ametoa muda wa miezi mitatu kwa wananchi waliovamia na kuanzisha shughuli za kibinadamu ndani ya Shamba la miti la Biharamulo kuondoka mara kwa hiari yao bila shuruti kabla ya mwezi Juni mwaka huu.

Ametoa muda huo ili wananchi waliolima mazao mbalimbali yakiwemo mahindi na pamba waweze kuvuna mazao yao kabla ya kuanza kwa oparesheni maalum ya kuwaondoa, iliyopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu itakayofanywa na Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania ( TFS) kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo.

Mhe.Kanyasu ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea shamba la miti Biharamulo lililopo katika wilaya ya Chato mkoani Geita.

Amesema Oparesheni hiyo haitasubiri taarifa ya Wizara tano inayoendelea kufanyiwa kazi kwa kuwa eneo hilo halihusiani na vile vijiji 366 vilivyokutwa ndani ya Hifadhi.

Amebainisha kuwa wananchi waliovamia eneo hilo wameitafsiri visivyo Kauli hiyo na kuongeza kuwa baada tu ya tamko la Mhe. Rais ,baadhi ya wananchi hata wale waliokuwa wakiishi katika maeneo mengine nje ya hifadhi waliendelea kuvamia na kuanza kujimilikishia maeneo makubwa wakidai kuhalalishwa na tamko la Rais.