Back to top

Kasha la risasi ya bunduki aliyoitumia Chifu Mkwawa kujiua lapatikana

15 December 2018
Share

Watafiti wa mambo ya kale kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam wamethibitisha kupatikana kwa kasha la risasi ya bunduki aliyoitumia chifu wa wahehe Mtwa Mkwawa kujiua kwenye eneo la Mlambalasi alikokuwa ameweka maficho yake wakati akipigana vita vya msituni dhidi ya wajerumani zaidi ya mika mia moja iliyopita.

Akitangaza rasmi ugunduzi huo mmoja wa watafiti hao dokta Frank Masele amesema ugunduzi wa risasi hiyo ya bunduki aina ya Mauser iliyotengenezwa ujerumani mwaka 1871 unathibitisha kuwa Mkwawa alijiua kwa kutumia silaha hiyo ya kijerumani ikiwa ni moja ya silaha zaidi ya mia tatu alizoziteka kwenye vita iliyogharimu maisha ya askari zaidi ya mia tatu wa ujerumani akiwemo kamanda wao Emil von Zelewski mwaka 1891.

Taarifa ya utafiti huo imetolewa katika kongamano la maonesho ya utalii ya karibu kusini yanayoendelea mjini Iringa huku watafiti wa chuo kikuu cha Iringa wakitangaza maeneo mapya matatu ya vivutio vya utalii yaliyotumika kuchimba na kufua chuma wakati wa vita vya Mkwawa dhidi ya wajerumani chuma kinachodhaniwa kilitumika kufua silaha zilizotumika na jeshi la Mkwawa.

Fatuma Mkwawa ni mwakilishi wa familia ya chifu Mkwawa anasema zipo taarifa nyingi kumuhusu Mtwa Mkwawa zilizohifadhiwa na familia lakini baadhi ya waandishi wa vitabu vinavyoelezea historia ya chifu Mkwawa wamezikosa kutokana na kushindwa kushirikisha familia hiyo.