Back to top

Kituo cha afya ikwiriri wilayani rufiji hakina huduma ya X-Ray.

24 June 2018
Share

Kituo cha afya ikwiriri wilayani rufiji hakina huduma ya X-Ray hali inayowalazimu wananchi kusafiri umbali mrefu kupata huduma hiyo katika hospitali ya wilaya ya Mkuranga huku baadhi ya wananchi wanaopatiwa huduma za afya katika kituo hicho wakilalamikia uchache wa dawa,ukosefu wa gloves wakilazimika kununua nje ya kituo hicho.

Wakipongeza hatua ya serikali kutoa shilingi Milioni 750 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa majengo mapya ikiwemo jengo la kuhifadhia maiti katika kituo hicho upanuzi wa wodi ya mama na watoto kituoni hapo  wananchi hao wameiambia ITV kuwa kituo hicho kinategemewa na wananchi wengi hivyo ni lazima huduma za dawa ziwepo kama ambavyo mmoja wa wananchi akielezea  kununua gloves kwa ajili ya kusafisha jeraha alilong'atwa na nyoka.

Msimamizi wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa kituo hicho Bw.Hussein Nassor unaotekelezwa kwa kuwashirikisha  wananchi kama utaratibu wa matumizi ya fedha zilizotolewa na serikali unavyoelekezwa amesema tayari majengo yamekamilika kwa asilimia kubwa.

Akizungumzia ujenzi na ukarabati wa kituo hicho Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mh Mohammed Mchengerwa amesema matokeo ya fedha zilizotolewa na serikali yameanza kuonekana kwa kituo cha afya Ikwiriri kubadilika na hadhi yake kuwa kama hospitali ya wilaya lakini amekiri  tatizo la X-Ray  na vifaa tiba ndio changamoto iliyobakia.