Serikali ya Tanzania na ile ya Jamhuri ya Korea zimekubaliana kushirikiana katika nyanja mbalimbali zikiwemo zile za afya na ujenzi lengo likiwa ni kuwafanya wakazi wa nchi hizo mbili kuweza kunufaika na ushirikiano uliopo baina ya mataifa hayo mawili.
Waziri mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amesema hayo Jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na waziri mkuu wa Jamhuri ya Korea Mhe. Mhe.Lee Nak-Yon na kuongeza kuwa baadhi ya matunda ya ziara hiyo ni Tanzania kunufaika na ujenzi mpya wa madaraja,barabara na hospitali za kisasa.
Waziri mkuu na mgeni walishuhudia hafla ya utiaji saini wa mkataba wa mahusiano ya kidiplomasia ambayo yanahusu uondoaji wa visa za kusafiria kwa wanadiplomasia na zile za utumishi yaliyofanywa na waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Dkt.Augustine Mahiga na makamu wa kwanza wa waziri wa mambo ya nje ya Jamhuri ya Korea Lim Sung –Nam.
Baadhi ya viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamesema ziara hiyo ni neema kwa Tanzania hasa katika taasisi wanazozisimamia kwani wanatumai mabadiliko chanya mengi yatakuwepo kutokana na mazungumzo yaliyofanyika.