Back to top

Korosho zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 160 zaibwa ghalani.

07 January 2021
Share

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linawashikilia watuhumiwa 14 kwa makosa mawili tofauti ikiwemo, tuhuma za kula njama, kuvunja ghala la korosho na kuiba gunia za korosho 1,515 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni miamoja na sitini mali ya Yalin Cashewnut Company. LTD.

Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Mark Njera amesema watuhumiwa tisa tayari wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuvunja ghala na kuiba korosho, huku watuhumiwa watano wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kosa la kupatikana na korosho zisizo na ubora.

Akizungumzia wizi wa korosho Kamanda Njera amesema kabla ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani walikiri kufanya kosa hilo eneo la maghalani manispaa ya Mtwara.

Amesema kabla ya kubainika kwa tukio hilo walinzi wawili wa Kampuni ya Fumwa Security Campany Limited waliacha kazi ghafla bila kutoa taarifa yoyote kwa viongozi wao huku wakijua makosa waliyoyafanya kwa kushirikiana na wenzao.

Hata hivyo walinzi hao wamekamatwa na kuhojiwa na kukiri kula njama na kushiriki kuiba korosho kwenye lindo walilokuwa na dhamana ya kulilinda kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya kazi yao.

katika tukio la pili kamanda Njera amesema wanawashikilia watu watano wakiwemo viongozi wa chama cha msingi cha Mwembe Tongwa kwa kosa la kukutwa wakiwa na korosho zisizo na ubora gunia miamoja na ishirini na nne.

kufuatia tukio hilo amesema upelelezi bado unaendelea na ukikamilika watuhumiwa wote watano watafikishwa kwenye vyombo vya sheria na ametumia fursa hiyo kuomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kukomesha matukio ya namna hiyo.