Back to top

Kundi la fisi latishia maisha ya wananchi mkoani Mara.

20 August 2018
Share

 
Hofu kubwa imetanda kwa wananchi wa kijiji cha Mika wilayani Rorya mkoani Mara baada ya kuibuka kwa kundi la fisi ambalo limekuwa likiwafukuza wakazi wa kijiji hicho hususani wanawake wanapokwenda visimani kutafuta huduma ya maji huku wakiomba serikali kuchukua hatua ya kukamilisha ujenzi mradi wa maji katika kijiji hicho ambao umedaiwa kujengwa kuanzia mwaka 2016 lakini umeshindwa kukamilika kwa madai ya ukosefu wa fedha.

Wananchi wa kijiji hicho cha mika wilayani Rorya, wametoa kilio hicho mbele ya Waziri wa maji na umwagiliaji Mh.Prof Makame Mbarawa, wakati akikagua miradi mbalimbali ya sekta ya maji katika wilaya hiyo, huku mbunge wa jimbo la Rorya Mh.Lameck Airo, akiomba serikali kumlipa mkandarasi suma JKT deni la shilingi milioni 42 ili aweze kuendelea na kazi hiyo na hivyo kuwaondolea wananchi adha hiyo.

Kwa upande wake Waziri huyo wa maji na umwagiliaji Mh.Prof Makame Mbarawa akizungumza na wananchi baada ya kukagua mradi huo katika kijiji cha mika amesema serikali itatoa fedha za kumlipa mkandarasi huyo haraka iwezekanavyo katika kumaliza changamoto hiyo,huku mkuu wa mkoa wa Mara Bw.Adam Malima akisema kushindwa kukamilika kwa mradi huo kwa wakati,kumesababisha kero kubwa kwa wananchi wa eneo hilo.