Back to top

Lugha ya Kiswahili yatangazwa kuwa rasmi ya 4 ya SADC

18 August 2019
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza uamuzi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kuwa lugha Kiswahili inakuwa lugha rasmi ya 4 ya SADC kuanzia leo tarehe 18 Agosti,
2019.

Mhe. Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo wakati akifunga Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika kwa siku 2 (tarehe 17-18 Agosti, 2019) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere
Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa uamuzi huo ni heshima kubwa kwa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye alitumia lugha ya Kiswahi katika harakati za ukombozi wa Mataifa mbalimbali ya Afrika hususani kwa wapigania uhuru ambao walijifunza na kutumia lugha hiyo katika mapambano dhidi ya wakoloni.

Amemuelezea Hayati Mwl. Nyerere kuwa alikuwa mtu mwenye huruma na upendo mkubwa sio tu kwa nchi yake ya Tanzania bali Afrika nzima kutokana na kujitoa kwake kwa hali na mali katika kusaidia mapambano ya ukombozi tena kwa gharama zilizobebwa na Watanzania.

Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wenzake walioshiriki mkutano huu wa 39 wa SADC Jijini Dar es Salaam kwa majadiliano yenye mafanikio makubwa waliyoyafikia, na ameeleza maazimio kadhaa yaliyofikiwa kuwa ni kuzitaka nchi wanachama kuendelea kutekeleza mkakati na mwongozo wa
maendeleo ya viwanda wa SADC wa mwaka 2015-2063, kuendelea kufuatilia hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kuitaka Falme ya Lesotho kuharakisha utungwaji wa sheria itakayoanzisha Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia mabadiliko na kuiagiza Sekretarieti ya SADC kuanzisha
chombo cha SADC cha kukabiliana na majanga.

Kuhusu hali ya uchumi, Mhe. Rais Magufuli amesema Wakuu wa Nchi na Serikali wamezitaka nchi wanachama kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha sera za uchumi na fedha.

Ameongeza kuwa wamejadili maombi ya Burundi kujiunga na SADC ambapo wameitaka Sekretarieti kuiarifu nchi hiyo juu ya maeneo ambayo bado hayajakamilika na kwa vikwazo dhidi ya Zimbabwe wamekubaliana kuendelea kuwasiliana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuondoa vikwazo hivyo huku wakisisitiza kuwa wapo pamoja na Zimbabwe.

Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Sekretarieti ya SADC kwa mchango wake katika maandalizi ya mkutano huo na ameitaka kutumia vizuri michango ya wanachama ili ilete matokeo katika ustawi wa jamii.

Amewakaribisha nchi wanachama wa SADC kuja kuwekeza nchini Tanzania na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.
Katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Mhe. Rais Magufuli, nchi 4 za SADC zitafanya uchaguzi Mkuu ambazo ni Malawi, Botswana, Mauritius na Msumbiji, hivyo amezitakia nchi hizo uchaguzi mwema wenye amani na utulivu.

Akimaliza muda wa mwaka mmoja wa Uenyekiti wake Mhe. Rais Magufuli atakabidhi Uenyekiti huo kwa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji mwezi Agosti
2020.

Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Ushelisheli Mhe. Danny Faure ambapo viongozi hao wamekubaliana kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano
kati ya Tanzania na Ushelisheli katika biashara na uwekezaji.

Mhe. Rais Magufuli amemualika Mhe. Rais Faure kuja kuwekeza katika viwanda vya samaki na kilimo na kwamba Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika.