Back to top

Mabasi 7 kati ya 38 ya abiria yameng'olewa namba za usajili Mwanza

19 April 2019
Share

Jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Mwanza, limefanya ukaguzi wa kushtukiza wa mabasi ya abiria yaendayo mikoani na nchi jirani katika kituo kikuu cha  mabasi Nyegezi pamoja na Buzuruga na kubaini mabasi saba yakiwa ni mabovu, huku madereva wakitozwa faini, magari yao kung'olewa namba za usajili na kuzuiliwa kuendelea na safari hadi hapo watakaporekebisha kasoro hizo.

Zoezi hilo lililoanza majira ya alfajiri, limeongozwa na kamanda wa polisi mkoa wa mwanza kamishna msaidizi wa polisi Muliro Jumanne Muliro.
Baadhi ya abiria pamoja na madereva wameeleza kufurahishwa na utaratibu huo.

Baada ya zoezi hilo lililofanyika sanjari na madereva kupimwa kilevi kuhitimishwa, kamanda wa polisi mkoani Mwanza kamishna msaidizi wa polisi Muliro Jumanne Muliro pamoja na mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani humo ACP Mkadamu Khamis Mkadamu wakatoa ushauri kwa abiria.

Jumla ya mabasi 38 ya abiria yamekaguliwa katika stendi mbili za Nyegezi na Buzuruga,lengo la ukaguzi huo wa kusthukiza ni kuhakikisha abiria wanaosafiri wanakuwa salama katika safari zao.