Back to top

Magufuli amtaka Mkurugenzi mpya TAKUKURU kushughulikia suala la rushwa

12 September 2018
Share

Rais Dkt.John Pombe Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu mpya wa Taasisi Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Kamishna wa Polisi Diwani Athumani kuongeza kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa nchini kwa kuhakikisha wote wanaokabiliwa na tuhuma za kujihusisha na rushwa wanafikishwa Mahakamani na sheria inachukua mkondo wake.

“Nataka ukaisafishe TAKUKURU, kuna baadhi ya wafanyakazi wa TAKUKURU wanajihusisha na rushwa, kawaondoe, nataka kuona TAKUKURU inashughulikia rushwa kwelikweli hasa rushwa kubwakubwa, ukipita huko vijijini wananchi wanateseka sana, wananyanyaswa na kuna dhuluma nyingi sana, na tatizo kubwa ni rushwa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mawaziri, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Satano Mahenge.

Viongozi walioapishwa ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) Dkt. John Kiang’u Jingu, Balozi wa Tanzania nchini Uganda Dkt. Aziz Ponary Mlima na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) CP Diwani Athumani Msuya.

Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Dkt. Jingu kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufuatilia usajili na utendaji kazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s), na kuhakikisha yanafanya kazi kwa kuzingatia sheria ambazo pamoja na mambo mengine zinayataka kuendesha shughuli zao kwa uwazi hususani masuala ya mapato na matumizi ya fedha za ufadhili wa shughuli zake.

Mhe.Rais Magufuli amemtaka Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Dkt. Mlima kusimamia vizuri ushirikiano wa Tanzania na Uganda hasa biashara na uwekezaji unaoendelea kati ya nchi hizi mbili na kuhakikisha Tanzania inanufaika na ushirikiano huo.

Viongozi walioapishwa na Mhe. Rais Magufuli pia wamekula kiapo cha uadilifu kwa watumishi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela na baada ya viapo vyao wamemshukuru Mhe.Rais kwa kuwateua na wamemuahidi kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.