Back to top

Magufuli amtwisha zigo Simbachawene utatuzi vibali NEMC kwa wawekezaji

22 July 2019
Share

Rais Dkt.John Pombe Magufuli amewaapisha Waziri wa Nchi Ofisi ya makamu wa Rais Mazingira Mhe. George Simbachawene na Naibu waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe katika Hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar Es Salaam.

Akizungumza baada ya kiapo cha Mawaziri hao, Dkt.Magufuli amemtaka Mhe.George Simbachawene kutatua changamoto ya ucheleweshaji wa vibali vya NEMC kwa ajili ya wawekezaji katika viwanda hapa nchini pamoja na kuhakikisha fedha zinazotolewa na wahisani kwa ajili ya mazingira zinaleta tija.

Aidha Amemtaka Naibu Waziri wa kilimo Mhe.Hussein Bashe kuhakikisha anatekeleza kwa vitendo tafiti na upembuzi aliyokuwa akiutoa bungeni kwa kuzingatia sekta ya kilimo ni muhimu na inachangamoto nyingi ikiwemo wizi ambapo ametolea mfano bodi ya sukari licha ya kufanya kazi nzuri lakini bado inapigwa vita na wafanyabiashara.

Awali akizungumza baada ya kuapishwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa rais Mazingira, Mhe. George Simbachawene ameahidi kushirikiana na watendaji wa wizara hiyo katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto ya rasilimali fedha toka kwa wafadhili kutumika katika shughuli za utawala zaidi badala ya kutatua changamoto ya mazingira.

Kwa upande Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe ameahidi kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya kilimo kwa kuzingatia asilimia 60 na 70 ya watanzania wanyonge na masikini wako katika sekta ya kilimo ambao wamekuwa wakilima kilimo cha kujikimu badala ya kilimo biashara.