Back to top

Mahakama kuu Musoma yasikiliza mashauri 18 kwa njia ya video.

13 May 2020
Share

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, imesikiliza jumla ya mashauri kumi 18 kwa njia ya Mahakama Mtandao ‘Video Conference’ tangu ilipoanza kutumia teknolojia hiyo Mei 5, mwaka huu.

 
Akizungumzia matumizi ya Mahakama Mtandao, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe, John Kahyoza alisema walianza kusikiliza mashauri mawili yote yakiwa yanayohusu maombi ya kukata rufaa nje ya muda yalisikilizwa mbele yake wakati wafungwa wakiwa katika gereza la Musoma bila ya wao kufika Mahakamani.

 
Jaji Kahyoza alifafanua kuwa   mashauri 10 yalisikilizwa mbele yake, manne  yalisikilizwa na Mhe, Jaji, Zephrine Galeba  na mashauri yaliyobakia  yalisikilizwa na  Mhe, Jaji Ephery  Kisanya.

 
Aliongeza kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma pia imeanza kusikiliza mashauri kwa njia hiyo Mei 12, mwaka huu, ambapo mashauri matatu yalisikilizwa  mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe, Rahim Mushi na kuaihirishwa bila ya Wakili wa Serikali Mhe, Jesse Temba na washtakiwa kufika mahakamani hapo.

 
Jaji Kahyoza alisisitiza kwamba Mahakama hiyo, itaendelea kusikiliza mashauri kwa mtandao. Pia itawekeana ratiba maalumu na Mahakama ya Hakimu Mkazi, zikiwemo za Wilaya ili kutekeleza maagizo ya viongozi wa juu wa Mahakama wakiwemo viongozi wa kitaifa wanaosisistiza kuepuka msongamano na mikusanyiko hasa katika kipindi hiki cha janga la Corona.