Back to top

Mahakama nchini Gibraltar yaamuru kuachiliwa meli ya mafuta ya Iran.

16 August 2019
Share


Mahakama ya juu nchini Gibraltar imetoa hukumu ya kuiachilia Meli ya mafuta ya Iran iliyokuwa imekamatwa nchini humo licha ya ombi la Marekani la kutotaka kitendo hicho kifanyike.

Hatua hiyo imekuja baada ya Gibraltar kupokea barua rasmi ya hakikisho kutoka kwa Iran kwamba meli hiyo haitapeleka mafuta yake nchini Syria.

Idara ya haki nchini Marekani iliwasilisha ombi kwa mamlaka nchini Gibraltar kuzuia kuachiliwa kwa meli hiyo ya Iran.

Meli hiyo kwa jina Grace 1 iliokuwa ikibeba mafuta ilikamatwa na wanamaji wa Uingereza tarehe 4 Julai hatua iliosababisha mgogoro na Iran.

Lakini Marekani iliomba taifa hilo kufikiria tena huku kesi yake ikitarajiwa kusikilizwa saa tisa muda wa Uingereza.

Meli hiyo ya mafuta ilikamatwa baada ya serikali ya Gibraltar kusema kwamba ilikuwa inaelekea Syria ikiwa ni ukiukaji wa vikwazo vya Muungano wa Ulaya.

Takriban wanamaji 30 walisafirishwa kutoka Uingereza kuelekea Gibraltar ili kuwasaidia maafisa wa polisi kuizuia meli hiyo ya mafuta na mizigo yake kufuatia ombi la serikali ya Gibraltar.