Back to top

Mahakama ya Kisutu kusikiliza maelezo ya mashahidi kesi ya Kitilya

08 February 2019
Share

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepanga kusikiliza maelezo ya mashahidi dhidi ya Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne, wanaokabiliwa na mashtaka 58 ikiwemo kula njama, kutakatisha fedha na kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani milioni sita.


Kadhalika, washtakiwa hao wanadaiwa kuongoza mtandao wa uhalifu, uliosababisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata hasara ya dola za kimarekani 600milioni.

Maelezo hayo yatasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Kesi hiyo ilipangwa kusikikizwa maelezo ya mashahidi  Feb 8 lakini wakili wa utetezi Dk. Masumbuko Lamwai alidai kuwa hawajapata nakala za maelezo hayo.

Dkt. Lamwai alidai kuwa utetezi unaomba nakala za maelezo hayo ili wayapitie kabla hawajasomewa washtakiwa.

Hakimu alisema upande wa Jamhuri utoe nakala kwa utetezi na kwamba washtakiwa watasomewa maelezo ya mashahidi Februari 12, mwaka huu.
Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine  katika kesi hiyo ni, Miss Tanzania wa 1996, Shose Sinare,  Sioi Solomon, aliyekuwa Kamishna wa Sera na Madeni kutoka Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda, (kwa sasa Ofisi ya Waziri Mkuu) na Alfred Misana, aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Sera na Madeni kutoka wizara hiyo (kwa sasa wizara ya afya).

Wote kwa pamoja wanakabiliwa na tuhuma ya uhujumu uchumi iliyopewa usajili namba 2/2019.

Katika mashtaka hayo mapya, mashtaka  49 ni  ya utakatishaji fedha, mashtaka matatu ya kughushi, moja la kuongoza Mtandao wa uhalifu, mawili ya kutoa nyaraka za uongo, shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanyanyifu, kula njama ya kutenda kosa kutumia  nyaraka kwa nia ya kumdanganya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.