Back to top

Majaji wa Mahakama ya rufani kusikiliza mashauri 38 Kagera.

20 August 2018
Share

Jumla mashauri 38 yatasikilizwa mkoani Kagera na kutolewa maamuzi na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya rufani Tanzania wakati wa kikao cha Mahakama hiyo kilichoanza leo mkoani humo ambacho kinafanyika kwenye jengo la Mahakama kuu kanda ya Bukoba kitakachomalizika Septemba 7, mwaka huu.

Ufunguzi wa kikao hicho umepambwa na Gwaride maalumu lililoandaliwa na kikosi cha jeshi la polisi katika mkoa huo ambalo limekaguliwa na mwenyekiti wa jopo la majaji hao Mhe.Jaji Mbaruk Salum Mbaruk.

Akizungumza baada ya ufunguzi wa kikao hicho Naibu msajili mwandamizi wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Elizabert Mkwizu amesema mashauri yatakayosikilizwa katika kikao hicho ni pamoja na mauaji, ubakaji, wizi na yanayohusiana na masuala ya madai naye mwenyekiti wa chama cha mawakili katika mkoa wa Kagera Aron Kabunga akizungumza uamzi wa serikali wa kusongeza huduma ya mahakama ya rufaa karibu na wananchi kuwa utaongeza wigo wa upatikanaji wa haki. 

Kwa upande wao baadhi ya wananchi katika mkoa wa Kagera waliozungumza kwa nyakati tofauti wamesema walikuwa wakipata usumbufu mkubwa katika kupata huduma ya mahakama ya rufani kwa kuwa walikuwa wakilazimika kuifuata jijini Mwanza jambo lililokuwa likiwagharimu fedha nyingi pia wameomba serikali iongeze idadi ya majaji ili haki kwa wananchi itolewe kwa wakati.