Back to top

Marekani kuwaondoa wanajeshi wake wanaohudumu nchini Afghanistan.

15 April 2021
Share

Rais Joe Biden wa Marekani amesema nchi yake itawaondoa wanajeshi wake wote wanaohudumu nchini Afghanistan ifikapo Septemba 11, siku hiyo ikiwa ni kumbukumbu ya miaka 20 tangu kufanyika kwa mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Marekani.

Ikulu ya Marekani imesema Biden ataweka wazi mipango yake juu ya Afghanistan na ratiba ya kuwaondoa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan katika hotuba yake.

Taarifa ya Ikulu imeongeza kuwa Biden atatembelea makaburi ya kitaifa ya Arlington ili kutoa heshima zake kwa wanajeshi waliofariki wakiitumikia nchi yao.

Uamuzi wa kuondoa wanajeshi hao ifikapo Septemba 11, umekuwa tofauti na muda wa mwisho wa Mei 1 uliofikiwa chini ya makubaliano ya amani na utawala wa Donald Trump na kundi la Taliban mwaka uliopita, lakini hautoi nafasi ya kuongeza muda huo.

Afisa mwandamizi katika utawala wa Biden amesema tarehe iliyowekwa sasa ya Septemba 11 ya kuwaondoa wanajeshi hao haiwezi kubadilika kutokana hali ya usalama nchini humo.