Back to top

Mawasiliano ya barabara yakatika baada ya daraja kuvunjika Dodoma.

24 May 2018
Share

Mawasiliano  ya barabara inayounganisha wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma na wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro yamekatika baada ya  kuvunjika kwa daraja la Godegode katika mto Ng'ombe linalounganisha wilaya hizo mbili kufuatia mvua za masika zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini na kupelekea wananchi kupata adha ya usafiri.

Akizungumza katika eneo la daraja hilo wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa barabara ya Mpwapwa naibu waziri wa ujenzi uchukuzi na mawasiliano Mhe. Elias Kwandikwa amesema serikali inaandaa taratibu za kuhakikisha mawasiliano kati ya vijiji hivyo yanarejeshwa.

Katika kuhakikisha mawasiliano yanarudi katika eneo hilo pamoja na maeneo mengine nchini naibu waziri Elias Kwandikwa amesema mkakati wa kuyashugulikia maeneo yaliyoathiriwa kipindi cha mvua za masika ikiwemo madaraja na barabara unashughulikiwa.

Baadhi ya wananchi wakiwemo wasafiri wakizungumza na ITV wamesema wanakabiliwa na adha kubwa kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha ambapo shughuli mbalimbali za kijamii zimesimama huku wakiiomba serikali kutafuta ufumbuzi wa kero hiyo.