Back to top

Maziko ya Dada wa Rais Magufuli, Monica Magufuli yafanyika Chato.

21 August 2018
Share

Rais Dkt.JOHN POMBE MAGUFULI amesema dada yake, Bibi MONICA JOSEPH MAGUFULI alikuwa mlezi wa mama yao mzazi, ambaye alimhudumia muda wote na kusema kwamba ameacha pengo kubwa katika familia yao.

Rais MAGUFULI amesema hayo alipokuwa akitoa shukrani kwa watu na viongozi mbali mbali waliohudhuria maziko ya dada yake, yaliyofanyika leo katika kijiji cha Lubambangwe, Chato Mkoa wa Geita.

Waliohudhuria maziko hayo ni pamoja na marais wastaafu watatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mabalozi, Mwakilishi wa Rais wa Burundi, Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya, Bwana RAILA ODINGA, Makamu wa Rais Mh.SAMIA SULUHU HASAN na Waziri Mkuu, Mh. KASSIM MAJALIWA .

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi JOHN KIJAZI, Naibu Spika wa Bunge , Dakta TULIA AKSON, Wakuu wa vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini, viongozi wa vyama vya upinzani Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na viongozi wa madhehebu ya dini.

Misa takatifu ya kumuombea marehemu MONICA JOSEPH MAGUFULI imeendeshwa na Askofu wa Jimbo la Ngara, Kanisa Katoliki,     Mhashamu SEVELINE NIWEMGIZI ambaye amewataka wafiwa kuwa wavumilivu kwa kuwa kifo hakivumiiliki kwa mwanadamu .

Awali akisoma wasifu wa marehemu kwa niaba ya familia ya MAGUFULI, Mkurugenzi ya Mawasiliano ya Rais - Ikulu- Bwana  GERSON MSIGWA amesema marehemu MONICA JOSEPH MAGUFULI amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza  wakati akitibiwa na kwamba marehemu amezaliwa mwaka 1955 ameacha mume, watoto tisa na wajukuu 25.