Back to top

Meli ya New Mv. Victoria yaanza safari za majaribio kwenda Bukoba

28 June 2020
Share

Meli ya New Victoria,Hapa Kazi Tu, ambayo ukarabati wake umekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 22.7, kwa ajili ya kuanza kutoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kati ya miji ya Mwanza na Bukoba, hatimaye hii leo imeanza safari zake za majaribio kutoka bandari ya Mwanza kwenda Bukoba ikiwa na abiria 292, wafanyakazi wa kampuni ya huduma za meli 60 na wakandarasi 58

Meli hiyo imeondoka katika bandari ya Mwanza kaskazini majira ya saa 2:55 asubuhi chini ya nahodha Bembele Samson Ng'wita ambaye pia ni meneja wa tawi la kampuni ya huduma za meli Mwanza kusini kuelekea bandari ya Bukoba.

Ukarabati wa meli hii, ulikuwa ni sehemu ya ukarabati mkubwa wa meli mbili ikiwemo ya Mv. Butiama ambayo itakuwa inafanya safari zake kati ya Mwanza na Nansio – Ukerewe.

Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Mwanza, ambaye ni mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cornel Magembe ambaye amesafiri na meli hiyo kwenda Bukoba amesema hakika rais Dkt. John Pombe Magufuli ametimiza ahadi yake kwa watanzania.

Katibu mkuu wa wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano sekta ya uchukuzi mhandisi Dkt.Leonard Chamriho ameshuhudia meli hiyo iliyosimama kufanya kazi tangu mwaka 2014, ikianza safari za majaribio.