Back to top

Merkel akiri Ujerumani kuathirika zaidi na virusi vya Corona.

19 March 2020
Share

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema Ujerumani ni moja ya nchi za Ulaya ambazo zimeathirika kwa kiasi kikubwa na virusi vya COVID-19.

Merkel ametoa kauli hiyo wakati wa hotuba yake na kusema nchi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia katika mapambano dhidi ya virusi vya corona ambapo pia amewasihi wananchi kuendelea kufuata maagizo yaliyotolewa na serikali ya kubakia majumbani na ametoa wito kwa taifa kuungana pamoja.

Siku ya Jumatano Ujerumani ilirekodi ongezeko la zaidi ya visa 1,000 vya virusi vya Corona ikilinganishwa na siku moja iliyopita, Kwa mujibu wa kituo cha utafiti cha John Hopkins, watu 12,300 wameambukizwa virusi hivyo nchini Ujerumani na wengine 28 wamekufa, huku zaidi ya watu 100 wakiwa wamepona.

Merkel amesisitiza kuwa hali ni mbaya na inapaswa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa kwani tangu kuungana kwa Ujerumani Mashariki na Magharibi, na tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Ujerumani haijawahi kukumbwa na changamoto kubwa kama ya mlipuko wa virusi vya corona, tofauti na nchi nyingine kama vile Italia, Ufaransa na Uhispania, Ujerumani haijaweka marufuku ya nchi nzima inayowazuia watu kuondoka majumbani isipokuwa kwa lengo la kwenda kazini, kupata matibabu au kununua chakula.