Back to top

Mfanyabiashara akutwa akijaza gesi kwenye mitungi kiholela, Moshi.

07 May 2021
Share

Mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia wa mtaa wa Hindu katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro  Bw.Dharmesh Velji amekutwa  akihamisha gesi kutoka kwenye mitungi mikubwa kwenda mitungi midogo ya wastani wa kilo sita hadi 15 kinyume cha sheria  katika mazingira hatarishi ikiwa imehifadhiwa kwenye gari bovu kama ghala lake.


Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Kilimanjaro Mkaguzi Abraham Ntezidyo amesema mfanyabiashara huyo na msaidizi wake  Bw.Hassani Amad wamekutwa na mitungi 173 ya ujazo mbali mbali ikiwemo yenye uzito wa kilo 38 kati yake 111 ikiwa na gesi na mingine 62 ikiwa haina kitu  chochote.
.
Aidha, Kaimu Meneja wa wakala wa vipimo mkoani Kilimanjaro Bw.Dennis Misango amesema, baadhi ya mitungi aliyokutwa nayo mfanyabiashara huyo ina ujazo sahihi lakini kosa lake ni kukutwa na vifaa vya kuhamishia na kujaza gesi kwenye mitungi karibu na makazi ya watu bila tahadhari yoyote.
.
Akizungumza na ITV kwa njia ya simu kutoka Arusha Meneja wa Wakala wa Nishati na Maji (EWURA) kanda ya kaskazini Mhandisi Lorivii Long' Idu amekiri baadhi ya makosa ya mfanyabiashara huyo na kumfungia biashara yake wakati hatua zingine za kisheria zikifuata.