Jeshi la Polisi Tanzania limewaonya watu wanaoingilia kazi za polisi katika upelelezi wa makosa mbalimbali kwa kulielekeza namna ya kufanya shughuli zake kwa ukamilifu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali wa Polisi SIMON SIRRO ametoa onyo hilo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kumpata mfanyabiashara maarufu nchini MOHAMMED DEWJI au 'MO', aliyekuwa ametekwa katika hoteli ya Collesium jijini Dar es Salaam Oktoba 11,2018 saa kumi na moja alfajiri alikokwenda kwa ajili ya mazoezi ya viungo.
Kamanda SIRRO amesema yeyote atakefanya hivyo atachukuliwa hatua stahiki bila kujali kama anafanya kwa faida yake au aliyemtuma.
Amewataka watu wenye mapenzi mema na taifa, wandelee kutoa ushirikiano katika upelelezi wa tukio hilo unaoendelea kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola hadi wahusika watakapokamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Akielezea mazingira ya kuachiwa kwa mfanyabiashara huyo leo saa kumi na moja alfajiri katika viwanja vya Gymkana, Kamanda SIRRO amesema polisi walikamata bunduki moja aina ya AK-47, bastola tatu pamoja na risasi kadhaa.