Back to top

Mgomo wa madereva daladala wakwamisha shughuli za kibiashara Dodoma.

19 August 2019
Share

Shughuli mbalimbali zimesimama kwa muda wa zaidi ya saa sita katika jiji la Dodoma kufuatia mgomo wa madereva wa daladala wakishinikiza kuondolewa wafanyabiashara waliovamia katika kituo kikuu cha daladala cha sabasaba kwa madai kuwa wamehodhi eneo kubwa na kuathiri shughuli na usalama wa usafiri huo wa umma.

Wakizungumza katika kituo hicho madeva na utingo wa daladala wanasema wameamua kugoma kutokana na msongamano wa wafanyabishara hatua wanayodai inaathiri shughuli zao huku wakihofia kutokea kwa majanga kutokana na matumizi holela ya moto yanayofanywa na wauza chipsi mama ntilie na wachoma mahindi.

Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara wanaolalamikiwa wanasema hawawezi kuondoka katika eneo hilo kwa madai kuwa shughuli zao zinafanyika kihalali kwani wana vitambulisho vya mjasiriamali na kuomba kuwe na utaratibu wa mgawanyo katika eneo hilo.

Kufuatia mgomo huo ikamlazimu mkurugenzi wa jiji la Dodoma Godwin Kunambi kufika eneo la tukio na kuwaamuru wafanyabiashara kuondoka kwa muda wakati wakitafutiwa utaratibu mwingine hatua iliyosaidia kumaliza mgomo huo na usafiri kurejea katika hali yake ya kawaida.