Back to top

Mhandisi apewa siku 14 kupeleka maji chuo cha ualimu Murutunguru.

09 August 2018
Share

Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella amempa siku 14 mhandisi wa maji wa wilaya ya Ukerewe William Kahurananga kuhakikisha ndani ya muda huo maji kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya ya chuo cha ualimu Murutunguru wilayani humo yanaanza kupatikana ili kuondoa changamoto ya vibarua kutembea umbali mrefu kusomba maji kichwani kwa ndoo ilikusudi ujenzi huo uweze kukamilika kabla ya mwezi oktoba mwaka huu.

Mongella ametoa agizo hilo baada ya kukagua ujenzi wa majengo ya chuo cha ualimu Murutunguru wilayani humo, kinachojengwa na serikali kupitia wizara ya elimu, sayansi na teknolojia kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5. Hii ni baada ya miundombinu ya chuo cha ualimu cha zamani kilichojengwa mwaka 1952 chenye uwezo wa kuchukua wanachuo 400 kuanza kuchakaa.

Mhandisi Kahurananga ameahidi kutekeleza agizo hilo kabla ya agosti 21 kwa kushirikiana na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Frank Bahati.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa John mongella amekabidhi vitabu 6,482 vya masomo ya hisabati, kiingereza, kiswahili, uraia na maadili, sayansi na teknolojia pamoja na maarifa ya jamii vilivyotolewa na serikali katika wilaya ya ukerewe.

Afisa elimu wa shule za msingi wilayani humo reginald richard, amesema idadi ya vitabu vilivyopokelewa vinaifanya wilaya hiyo kuwa na jumla ya vitabu 38,891 na hapa anaeleza changamoto ya vitabu hasa kwa wanafunzi wa darasa la nne ilivyokuwa huko nyuma.

Nao baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi na maafisa elimu kata wilayani humo wameahidi kuvitunza vitabu hivyo na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuinua kiwango cha ufaulu katika wilaya hiyo.

 

 

 

.