Back to top

Mhe.Biteko atatua mgogoro wa muda mrefu katika mgodi wa Maganzo

11 December 2019
Share

Hatimaye serikali kupitia wizara ya madini imetatua mgogoro wa muda mrefu uliokuwa ukifukuta kati ya wachimbaji wadogo wa madini ya Almasi wa eneo la Maganzo wilayani Kishapu na uongozi wa mgodi wa Almasi wa Wiliamson diamond (WDL)kwa kuagiza mabaki ya mchanga uliochenjuliwa madini utolewe nje ya eneo la mgodi na kupewa wananchi kwa lengo la kuufanyia marudio.


Agizo hilo limetolewa na waziri wa madini Dotto Biteko wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya Almasi katika eneo la Maganzo wilayani Kishapu na kudai kuwa serikali imesikia kilio na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wanaozunguka mgodi wa Williamson diamond LTD (WDL) ya kunyimwa mabaki ya mchanga uliochenjuliwa madini hali ambayo imekuwa ikisababisha migongano na migogoro ya mara kwa mara.


Nao baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya Almasi wa eneo hilo la Maganzo wamesema uamuzi wa serikali ni fursa kwao ya kujijenga kiuchimi na kuahidi kulipa kodi ya serikali kwa wakati.


Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa shinyanga bi.zainab telack amesema uongozi wa mgodi wa alimasi wa mwadui umeridhia kushirikiana na serikali kujenga soko la kisasa la madini ya alimasi katika eneo la maganzo ili kuwarahisishia wachimbaji wadogo kuuza alimasi zao huku mbunge wa kishapu selemani nchambi akidai kuwa mchanga huo sasa ni fursa ya ajira kwa vijana na wanawake waliokuwa wanahangaika muda mrefu bila mafanikio.